Posted by : FURAHA MEDIA
Wednesday, April 6, 2016
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limezindua kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Songosongo wilayani Kilwa mkoa wa Lindi chenye uwezo wa kupokea futi za ujazo milioni 70 kwa siku kutoka kwenye visima na kwa kuanzia kitapokea futi za ujazo milioni moja.
Kwa sasa wanafanya majaribio hadi kufikia Juni 30, mwaka huu futi zote za ujazo milioni 70 zitakuwa zimeungana na gesi inayotoka Mnazi Bay katika eneo la Somangafungu na kuanza kusafirishwa kwa bomba la gesi kwenda jijini Dar es Salaam.
Akizindua mtambo huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, alisema kufikia Juni 30, mwaka huu bomba la gesi litasafirisha gesi ya futi za ujazo bilioni 10.27 kwenda jijini Dar es Salaam.
Dk Mataragio alisema mitambo ya Songosongo ina uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 140 katoka visima vinne na Kisima cha Kiliwani -North kitatoa gesi futi za ujazo milioni 20 hadi 30 kwa siku.
“Kwa kuwa mitambo yetu bado ni mipya kitaalamu hatuwezi kuingiza gesi nyingi kwa wakati mmoja, hivyo gesi huingizwa katika mitambo kidogo kidogo kupima uwezo wake lakini mpaka mwezi Juni gesi yote itakuwa imefika jijini Dar es Salaam kwa kutumia bomba la gesi,” alisema Dk Mataragio.
Alisema majaribio yanafanyika ili kupima uwezo wa mitambo kuhimili kiwango cha gesi inayoingia na kuichakata katika viwango vinavyotakiwa na ujazaji wa gesi kwenye bomba na kupima mgandamizo wa gesi.
Pia kuisukuma kwenda Somangafungu ambapo itakutana na ile inayotoka Madimba na kisha kuweka katika mgandamizo sawa na kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Dk Mataragio alisema mitambo hiyo ya kuchakata gesi ya Songosongo inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 100, kwa sasa itakuwa ikipokea gesi kutoka katika vitalu viwili ambavyo ni Kiliwani inayomilikiwa na Ndovu Resources na Songosongo inayomilikiwa na Pan African Energy Tanzanie-PAET.