Posted by : FURAHA MEDIA Monday, May 2, 2016

Na Saleh Ally
MPIRA wa Tanzania umejaa mambo mengi sana yanayohusiana na suala la ubinafsi, ushabiki usio na tija na watu wengi sana kutopenda au kukubali kuambiwa ukweli.
Ukiwaeleza watu ukweli, wanakuona adui namba moja, huenda wakaanza kutafuta makosa yako au kulazimisha makosa wapate nafasi ya kuionyesha jamii nawe ni mkosaji.

Ukosaji wa mtu mwingine, hauwezi kuidhinisha udhaifu kwenye jambo la maendeleo ya jamii katika michezo. Vizuri anayekosea umsaidie afanye vizuri ili wote mfanye vizuri, ndiyo maana lengo ni kukosoa.

Unakumbuka, Simba ilifanya biashara ya kumuuza Emmanuel Okwi mwaka 2013, nikasema ilikuwa biashara kichaa kwa kuwa kiongozi wa Simba wakati huo, Ismail Aden Rage hakuwa makini na alikurupuka.


Baada ya Simba kulipwa mwaka 2016, huenda kiongozi huyo anaona ni wakati wa kutaka kuonyesha wengine hasa waliomuambia alikosea ndiyo wamekosea. Najua kamwe hawezi kupata sehemu tuliyosema au niliyosema alikula fedha, kwa kuwa sikuwa nimewahi kusikia amezila.

Msisitizo unabaki palepale, Simba walifanya biashara hiyo ‘kichaa’. Okwi aliuzwa Etoile du Sahel, akaenda SC Villa ya Uganda, baadaye Yanga, karudi Simba, kote biashara inafanyika. Simba wakamuuza Ulaya, bado wao hawakuwa wamelipwa fedha za biashara ya kwanza. Hiyo ndiyo biashara kichaa na nikisikia kelele zaidi, nitakwenda ndani siku moja nichambue zaidi kwa nini biashara hiyo ni kichaa.
Leo, ninalalia kwenye jambo ambalo nimeendelea kulikumbushia kila mara. Klabu kubwa za Yanga na Simba kukosa hata viwanja vya mazoezi miaka nenda rudi na ajabu kabisa, hakuna kiongozi ambaye ameziongoza na akaona aibu hata kidogo.

Sasa zina viongozi wa juu wasomi na vijana. Simba wana Evans Aveva na Yanga wana Yusuf Manji. Wote ni wafanyabiashara ingawa Manji ni mfanyabiashara mkubwa zaidi. Je, hawaoni vibaya au hawajisikii vibaya kuona wachezaji wao wakifanya mazoezi kwenye viwanja vya kukodi?


Hawaoni vibaya kuona klabu ya daraja la nane Ulaya inakuwa na kiwanja na klabu kubwa kama Yanga au Simba ambayo wakati mwingine inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika au kimataifa, inashindwa kuwa na uwanja wa mazoezi tu?

Kama Manji na Aveva wanashindwa, watu wenye mawazo ya biashara na vijana wa kisasa, nani ataweza au ugumu wa hili uko wapi?

Kilichonikumbushia hili ni baada ya kuona picha ya kipa Vincent Angban wa Simba akiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Mlalakuwa, Kawe jijini Dar es Salaam.
Kipa huyo akiwa mazoezini, anasubiri kupigiwa au kurushiwa mpira huku mtu mwingine akifanya kazi ya kutoa maji uwanjani. Anayamwaga kwa kuwa nyuma alipo kipa huyo kuna dimbwi kubwa la maji.
Ndiyo mvua zinanyesha, lakini kwa kuwa viwanja wanavyotumia pia ni hovyo kabisa, ndiyo maana inalazimika kufanyika huduma kama hiyo ya aibu katika soka ya Tanzania. Ninaamini yeyote aliye Misri, Rwanda, Algeria, Afrika Kusini na kwingineko akiona picha hiyo na kuambiwa Simba wako mazoezini, lazima atashangazwa na hilo.
Lakini vipi viongozi wa Simba wenyewe hawashangazwi au kuumizwa nalo? Kuna maneno mengi ya kujitetea lakini klabu hizi kongwe na nyingine ambazo hazina viwanja lazima wakubali soka nchini linafeli kwa kiwango kikubwa na viwanja ni moja ya sehemu.

Kwani haya walio na viwanja vyao kama Mtibwa Sugar, zikinyesha mvua kidogo tu ni shida. Tunaona wenzetu mvua zinanyesha na mechi zinachezwa pia.

Heshima ya uwanja wa kuchezea ni kubwa sana katika nchi zote zilizopiga hatua kimaendeleo kisoka. Wanajua pale ndiyo kila kitu na lazima mkubali, soka haina burudani sahihi kama uwanja ni mbaya.
Utawasikia Yanga na Simba wanachekesha kwa kusema wanakwenda kucheza mikoani kuna viwanja vibovu na ndiyo hofu yao ya kupoteza michezo.
Wao wana viwanja vizuri? Vipi au wapi? Ule wa Taifa ambao ni wa serikali? Kwani ni wao? Sasa wanachozungumza hasa ni kipi!
Picha hiyo ya Angban, inaonyesha namna gani mazungumzo, mipango na hata mavazi yetu yalivyo ya karne hii tena mwaka 2016. Lakini usahihi na uhalisia, bado tumebakizwa mwaka 1935 na 1936 wakati Yanga na Simba zinaanza.
Viongozi wa wakati ule, waliokuwa masikini, walioishi miaka ya 1900 ndiyo walikuwa bora na wenye akili na malengo sahihi. Ndiyo maana Yanga na Simba zinajivunia nyumbani hii leo. Zina sehemu au makao makuu.
Hawa wa sasa ambao walitakiwa kuendeleza tu, wamekwama. Kila anayeingia ana hadithi yake mpya na aibu inaendelea kurundikana.

Lazima Yanga na Simba waendelee kuelezwa katika hili. Najua siku wakiamua kujirekebisha, basi wataona kama wamewashinda ‘waovu’ waliokuwa wanawaeleza ukweli. Maneno mengi, myaache yatungiwe nyimbo na utendaji uchukue nafasi yake kuusaidia mpira wa Tanzania kama ambavyo wazee walioachia majengo walifanya, nanyi tendeni, hadithi na aibu hii sasa basi, eeeh!

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © FURAHA MEDIA - Blogger Templates - Powered by Blogger - Designed by Johanes Djogan -